☞ Tarjama na faida katika Surat al-Ikhlaas;
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ.
Kwa majina ya Allah mwingi wa Rahma na Mwenye kurehemu.
قُلْ هُوَ اللّٰهُ أَحَدٌ ﴿١﴾ اللّٰهُ الصَّمَدُ ﴿٢﴾ لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُوْلَدْ ﴿٣﴾ وَلَمْ يَكُنْ لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ ﴿٤﴾
1 – Sema: Yeye Allah ni mmoja tu.
2 – Allah ndiye mwenye kukusudiwa.
3 – Hakuzaa na wala hakuzaliwa.
4 – Na hakuna hata mmoja anayefanana naye.
Maelezo ya Mfasiri:
Allah amejikanushia yeye mwenyewe kuwa hakuzaa na mtoto hutokana na baba na ni sehemu katika mwili wake na Allah – aliyetukuka – hana mfano.
Na vile vile mwanadamu humuhitajia mtoto kwa sababu ya haja aliyokuwa nayo katika msaada wa kidunia au kwa ajili ya kuendeleza kizazi na Allah – aliyetukuka – amejitosheleza na hilo, na kuzaa kuna hitaji mke na Allah – aliyetukuka – ametakasika na hilo. Na katika aya hii inabainisha upotevu wa makundi matatu:
1 – Washirikina wa kiarabu waliodai kuwa Malaika na watoto wa kike wa Allah – ametakasika na hilo kabisa.
2 – Mayahudi waliosema kuwa Uzair ni mtoto wa Allah – ametakasika na hilo kabisa.
3 – Manaswara (Wakristo) ambao wamesema kuwa Issa (Yesu) bin Mariam ni mtoto wa Allah – ametakasika na hilo kabisa. Na vile vile Allah hakuzaliwa kwa sababu yeye ndiye wa kwanza (wa mwanzo) ambaye hana mwanzo na kabla yake hakukuwepo chochote hii ina maana hakuzaliwa.
Sura hii ina fadhila nyingi katika fadhila zake imethibiti kutoka kwa Mtume – swala na salamu za Allah zimfikie – kuwa sura hii inafanana na theluthi (moja ya tatu) ya Quran, na wanachuoni wakaeleza kuwa sura hii inalingana na theluthi ya qurani kwa sababu maana ya aya za Qur’ani imegawanyika sehemu tatu:
1 – Tauhidi; yaani kuna aya zinazozungumzia masuala ya kumpwekesha Allah na imani.
2 – Hukumu; kuna aya zinazozungumzia hukumu mbalimbali kama, swala, zaka, n.k
3 – Visa; visa mbalimbali vya mitume waliopita na mataifa yao .
Na katika sura hii kuna sifa za Allah kwa hiyo sura hii imehusishwa kwa tauhidi tu ndiyo maana ikawa inalingana na moja ya tatu ya quran. Na sura hii Mtume – swala na salamu za Allah zimfikie – alikuwa akiisoma katika rakaa ya pili ya suna ya rakaa mbili kabla ya al-fajir na pia katika rakaa ya pili ya rakaa mbili baada ya swala ya magharibi, na pia alikuwa akiisoma katika rakaa ya mwisho ya witri. Vile vile sura hii katika kujikinga inasomwa pamoja na suratul-falaq na suratu nnas mara tatu tatu asubuhi na jioni na pia wakati wa kulala mara tatu tatu pamoja na kutemea vijimate katika katika viganja na kujipaka mwili mzima. Hii ndiyo kinga ya kisheria. Mwisho: Na Sura hii Allah – aliyetukuka – ameihusishia nafsi yake kwa sababu hakuna kilichotajwa ndani yake isipokuwa ni majina yake na sifa zake na mtu mwenye kuisoma sura hii hali ya kuiamini na hali ya kuitakidi yale yaliyojulishwa na sura hiyo basi bila shaka mtu huyo – ni mwenye kumtakasia ibada Allah na amesalimika na ushirikina.
Mfasiri: fawaidusalafiya.net
Imeandaliwa: Tarehe 09 – Rabi’u-Awwal – 1442H ≈ 26 – October – 2020M.
Tembelea website yetu: ⇩⇩ https://www.fawaidusalafiya.net
Kupata faida nyingi ungana nasi Telegram kwa kubonyeza link hii: https://t.me/fawaidussalafiyatz
Kupata darasa za ndoa jiunge nasi Telegram kwa kubonyeza link hii: https://t.me/Darasazandoa
Jiunge nasi: Instagram, Twitter, facebook na you tube: @fawaidusalafiyatz
#Muhimu: Vuna thawabu kwa kusambaza faida hizi. Sambaza kama ilivyo, si ruhusa kubadilisha chochote. Tuwe waadilifu. •┈┈┈┈••✦✿✦••┈┈┈┈•