Makala namba (32)
قال تعالى عن الملك :
Amesema (Allah) aliyetukuka – kuhusu mfalme :
وَقَالَ ٱلْمَلِكُ ٱئْتُونِى بِهِۦ ۖ فَلَمَّا جَآءَهُ ٱلرَّسُولُ قَالَ ٱرْجِعْ إِلَىٰ رَبِّكَ فَسْـَٔلْهُ مَا بَالُ ٱلنِّسْوَةِ ٱلَّٰتِى قَطَّعْنَ أَيْدِيَهُنَّ ۚ إِنَّ رَبِّى بِكَيْدِهِنَّ عَلِيمٌ
Na mfalme (alipopelekewa habari hii) alisema : “Mleteni kwangu ”. Basi mjumbe alipomjia (Yusufu) , alisema (Yusufu) : Rejea kwa bwana wako ukamuulize khabari ya wale wanawake waliojikata mikono yao; bila shaka Mola wangu Mlezi anazijua sana hila zao.
سورة يوسف ٥٠
Maelezo ya muandishi :
Yule mtu pindi aliporudi kwa mfalme na akamuelezea ile tafsiri ya ndoto kutoka kwa Yusufu ,basi mfalme akapendezewa na Yusufu na akamwona kuwa atakuwa na faida naye, na akaazimia amuite. Akawaamrisha wasaidizi wake wamlete .
Alipomfikia mjumbe akamwambia kuwa mfalme anamtaka,Yusufu akamwambia mjumbe : Rejea kwa bwana wako mwambie akawaulize wale wanawake waliojikata mikono waelezee uhalisia wa yale waliyonifanyia, na hapa Yusufu hakuweka wazi katika mazungumzo yake kuwa wanawake hao walimtaka afanye nao machafu bali alitumia fumbo .
Na Yusufu -amani iwe juu yake -alisema kuwa :
“Bila shaka Mola wangu Mlezi anazijua sana hila zao ” .
Anakusudia vile vitimbi na hila walizomfanyia hao wanawake kama alivyoeleza Allah -aliyetukuka -pale aliposema kuhusu yule mwanamke wa waziri mkuu :
وَآتَتْ كُلَّ وَاحِدَةٍ مِّنْهُنَّ سِكِّينًا وَقَالَتِ اخْرُجْ عَلَيْهِنَّ ( ٣١)
Na akampa kila mmoja katika wao (wanawake) kisu na akamwambia (Yusufu), “Tokeza mbele yao”.
Hapa tunapata faida namna Yusufu alivyokuwa na subira ya hali ya juu kwa sababu ile habari aliyoletewa haikumpapatisha, juu ya kuwa ina bishara ya kufunguliwa kwake.
Wala hakuwa kama vile mfungwa anayetamani kutoka katika hali yenye dhiki za jela na taabu zake hilo halikuitikisa subira yake.
Yusufu akakhiari angoje mpaka idhihirike kuwa hana makosa kuliko kufanya haraka kutoka na huku yale aliyotuhumiwa bado yamemganda.
Yusufu alitaka kutoka gerezani utokaji wa yule ambaye imethibiti kuwa hana makosa na wala si utokaji wa yule aliyesamehewa.
Ndiyo maana Mtume -swala na salamu za Allah zimfikie -alimsifu nabii Yusufu -amani iwe juu yake -kwa subira ya hali ya juu aliyokuwa nayo akasema :
ولو لَبِثْتُ في السِّجْنِ طُولَ ما لَبِثَ يُوسُفُ، لَأَجَبْتُ الدَّاعِيَ.
“Na lau ningekaa gerezani (muda) mrefu kama alivyokaa Yusufu basi ningemjibu (yule) aliyekuja kuniita (nitoke) ”
رواه البخاري
Tanbih :
Hadithi hii haijulishi kuwa Yusufu -amani iwe juu yake – yeye ni mtukufu kuliko Mtume -swala na salamu za Allah zimfikie -,lakini Mtume -swala na salamu za Allah zimfikie -alitaka kubainisha subira yake Yusufu -amani iwe juu yake -na kubainisha unyenyekevu wake Mtume -swala na salamu za Allah zimfikie – pamoja na kuwa kwake ni mbora zaidi ya Yusufu lakini alimsifu kwa subira aliyokuwa nayo.
Bila shaka kifungo alichofungwa Mtume -swala na salamu za Allah zimfikie – yeye na watu wake mwanzoni mwa Uislamu ni kifungo kizito zaidi ya kifungo cha watu hawa kwa Yusufu , kwa sababu hao washirikina waliomzuia Mtume -swala na salamu za Allah zimfikie -walikubaliana kuwa wasiwaozeshe na wala wasiwauzie yaani Mtume -swala za Allah zimfikie -na watu wake.
Pia tunapata faida kuwa kifungo hakishushi daraja la mtu :
Yusufu -amani iwe juu yake -alifungwa hali ya kudhulumiwa.
Imam Ahmad -Allah amrahamu -alifungwa hali ya kudhulumiwa.
Ibn Taimiyyah -Allah amrahamu-alifungwa hali ya kudhulumiwa.
Na tunaona kuwa Yusufu pamoja na kuwa alifungwa kwa dhulma lakini hakuacha kulingania humo gerezani kama alivyowalingania wale wafungwa :
يَٰصَىٰحِبَىِ ٱلسِّجْنِ ءَأَرْبَابٌ مُّتَفَرِّقُونَ خَيْرٌ أَمِ ٱللَّهُ ٱلْوَٰحِدُ ٱلْقَهَّارُ (٣٩)
“Enyi wafungwa wenzangu wawili!Je!Waungu wengi wanaofarikiana ndio bora (kuabudiwa) au Allah Mmoja Mwenye nguvu (juu ya kila kitu ?)”.
سورة يوسف
Na hapa tunajifundisha kuwa muislamu haachi kulingania hata akiwa katika hali ya dhiki na shida.
Muandishi : Abuu Thurayyaa Ismail Seiph Mbonde Asshafiy .
Muandaaji: fawaidusalafiyatz.net
Tembelea website yetu: ☟
https://www.fawaidusalafiyatz.net
Telegram bonyeza hapa: ☟
https://t.me/fawaidussalafiyatz
🗓️ Imeandaliwa: Mfungo tatu 24, 1443H ≈ Jul 23, 2022M.
Muhimu: Vuna thawabu kwa kusambaza faida hizi. Sambaza kama ilivyo, si ruhusa kubadilisha chochote. Tuwe waadilifu.
Jiunge na chennel yetu ya telegram upate faida nyingi, kujiunga bonyeza link hii: 👇🏾
https://t.me/fawaidussalafiyatz
•┈┈┈┈•✿❁✿•┈┈┈┈•