Hukumu ya kuuza vyakula mchana wa Ramadhani na aina ya vyakula

Makala namba: 1

Vyakula vimegawanyika sehemu mbili:

1 – Vyakula ambavyo dhana yenye nguvu inahukumu kuwa mnunuzi atakula muda ule ule kwa sababu ya sifa ya hicho chakula na haja yake mfano wa vyakula hivyo ni: icecream, soda, juisi, na vinywaji baridi au vya moto, mihogo ya kukaanga, chips, wali, ugali, yaani vyakula vinavyouzwa hali ya kuwa vimeshapikwa, na pia kufungua migahawa, mahoteli, n.k:

Hukumu ya kuuza biashara hizi haifai mchana wa Ramadhani kwa sababu dhana yenye nguvu ina hukumu kuwa wanunuzi wa vyakula hivi watavunja utukufu wa mwezi wa Ramadhani kwa kula mchana na haifai kuuza vyakula hivi sawa sawa kwa waislamu au makafiri, kwa sababu kufanya hivyo ni kuwasaidia juu ya madhambi, Allah amesema:

(وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَى وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ وَاتَّقُوا اللَّهَ إِنَّ اللَّهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ)

{ Na saidianeni katika wema na uchamungu. Na wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Allah.Hakika Allah ni mkali wa kuadhibu.

المائدة : ٢

Na amesema Sheikh ibn Uthaimin – Allah amrahamu:

“لا يجوز فتح المطاعم ولو للكفار -وطبعاً للمسلمين غير مفتوحة- في أيام رمضان، ومن رأى منكم صاحب مطعم فتحه في رمضان وجب عليه أن يبلغ الجهات المسئولة لمنعه، ولا يمكن لأي كافر أن يظهر أكلاً أو شرباً في نهار رمضان في بلاد المسلمين، يجب أن يمنع من ذلك”

” Haifai kufungua migahawa kwa ajili ya makafiri – ndio kwa waislamu haifunguliwi – katika (mchana) wa Ramadhani na yeyote miongoni mwenu atakayemuona mwenye mgahawa ameufungua mgahawa wake (mchana) wa Ramadhani ni wajibu awafikishie wale wenye majukumu (serikali) ili wamzuie na wala haiwezekani kwa kafiri yeyote kudhihirisha kula au kunywa katika mchana wa Ramadhani katika miji ya kiislamu inawajibika azuiliwe kutokana na hilo.

” اللقاء الشهري ٤ /٨، بترقيم الشاملة آليا)

Maelezo ya mfasiri:

Kuhusu uharamu wa kuwauzia makafiri vyakula vinavyoliwa mchana:

Amesema Allah – aliyetukuka – pindi alipowazungumzia watu wa peponi, akasema kuwa watu wa peponi watawauliza watu wa motoni:

مَا سَلَكَكُمْ فِي سَقَرَ (٤٢) قَالُوا لَمْ نَكُ مِنَ الْمُصَلِّينَ (٤٣) وَلَمْ نَكُ نُطْعِمُ الْمِسْكِينَ (٤٤) وَكُنَّا نَخُوضُ مَعَ الْخَائِضِينَ (٤٥) وَكُنَّا نُكَذِّبُ بِيَوْمِ الدِّينِ (٤٦) حَتَّى أَتَانَا الْيَقِينُ (٤٧)

Ni lipi lilowaingiza Motoni?
Watasema: Hatukuwa miongoni mwa walio kuwa wakiswali. Na hatukuwa tukiwalisha masikini. Na tulikuwa tukizama pamoja na waliokuwa wakizama (katika maovo). Na tulikuwa tukiikanusha siku ya malipo. Mpaka tukajiwa na kifo.

سورة المدثر ٤٢-٤٧

Ufafanuzi:

Hii aya ni dalili kuwa Makafiri wanalazimika kutekeleza matawi ya sheria kama vile kuswali, kufunga, kutoa zaka na mengineyo na ndio maana siku ya kiama wataadhibiwa kwa kutotekeleza hayo kama tulivyoona katika aya hizi.

Kwa hiyo kama kafiri anawajibika kufunga Ramadhani, basi ni haramu kumuuzia au kumpa chakula ambacho unajua kuwa atakila mchana wa Ramadhani, au dhana yako yenye nguvu inajua kuwa atakila mchana wa Ramadhani yaani vile vyakula ambavyo mnunuzi huvila muda ule ule.

Ni vipi kafiri awajibike kufunga hali ya kuwa hajaingia katika uislamu?

Jawabu: Kwanza anatakiwa aondoe kizuizi cha kukubaliwa hiyo ibada yaani aingie katika uislamu kisha afunge.

Ama wale ambao sheria imewaruhusu kula basi hakuna ubaya kuwauzia kama vile: Wagonjwa, wasafiri, watoto, n.k

Inaendelea .. usikose namba 2.

Comments

No comments yet. Why don’t you start the discussion?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *