MAZINGATIO KATIKA KISA CHA NABII YUSUFU-AMANI IWE JUU YAKE-

https://t.me/fawaidussalafiyatz

Website ingia hapa: https://www.fawaidusalafiya.net

MAZINGATIO KATIKA KISA CHA NABII YUSUFU -AMANI IWE JUU YAKE- .

Makala namba (15) .

قال تعالى :

Amesema (Allah) aliyetukuka-:

وَلَمَّا بَلَغَ أَشُدَّهُ آتَيْنَاهُ حُكْمًا وَعِلْمًا وَكَذَلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ (٢٢)

{Na (Yusuf) alipofikia utu uzima tulimpa hukumu na elimu .Na kama hivi tunawalipa wanaotenda mema .

وَرَاوَدَتْهُ الَّتِي هُوَ فِي بَيْتِهَا عَنْ نَفْسِهِ وَغَلَّقَتِ الْأَبْوَابَ وَقَالَتْ هَيْتَ لَكَ قَالَ مَعَاذَ اللَّهِ إِنَّهُ رَبِّي أَحْسَنَ مَثْوَايَ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الظَّالِمُونَ ( ٢٣)

Na (yule mwanamke) wa nyumba aliyokuwamo Yusufu,alimtaka (Yusufu) kwa upole na kubembeleza;na akafunga milango ,na akamwambia , “Njoo” (Yusuf) akasema: “Najikinga kwa Allah.Hakika huyo (mumeo) ni bwana wangu, ameyafanya mazuri mashukio (makazi) yangu .Hakika hali ilivyo madhalimu hawafaulu .
(23)

Maelezo ya muandaaji:

Pindi alipofikia umri wa utu uzima yaani karibu na miaka arobaini Allah alimpa hekima yaani ufahamu na kupatia katika maneno anayoyazungumza na matendo anayoyatenda na yote hayo yaliambatana na kupewa elimu na pia alipewa utume.

Hapa tunajifunza kuwa mwanachuoni anahitajia hekima ambayo ni kuweka kila jambo sehemu yake kwa kuangalia lengo zuri ukomo mzuri katika hilo, kwa ajili hii unaweza ukamuona mtu ana elimu lakini hana hekima ,na kuna wengine wana hekima katika baadhi ya vitu lakini hawana elimu ,kwa hiyo ukamilifu ni mtu kupewa : Elimu na hekima .

Mwisho wa aya Allah -aliyetukuka- akasema kuwa kama alivyomlipa Yusufu kutokana na wema wake basi hivyo hivyo ndivyo anawalipa watu wenye kufanya mema mpaka kiama .

Aya inayofuata : Inasimulia mtihani wa pili aliopewa Yusuf nao ni mtihani wa matamanio na huu ni mtihani mzito mno kwa Yusuf -amani iwe juu yake- kuliko mtihani uliopita baina yake na ndugu zake kama walivyoeleza baadhi ya wanachuoni , na mtihani huu wa huyu mwanamke ulikuwa mkubwa zaidi kwake kwa kuzingatia kuwa yeye alikuwa ni :

Barobaro (kijana),
Hajaoa ,
Mwanamke aliyemtaka ni mke wa kiongozi mkubwa mwenye cheo na ana mali, vilevile tendo hili la kumtaka lilifanyika katika nyumba ya huyu mwanamke yaani hakuna mashaka ya kutuhumiwa hata kidogo ,na huyo mwanamke ndiye aliyemuita Yusufu ,na alijiandaa kwa ajili yake Yusuf kwa kujipamba na kujiremba ,na alifunga milango yote sawa sawa yaani kwa uimara na hakubakisha hata mlango mmoja kuwa wazi ,na mumewe alikuwa hayupo,lakini pamoja na wepesi wa kufanyika jambo hili Allah -aliyetukuka- alimpa msaada Yusuf na akamthibitisha na akamuongoza katika kheri na Yusufu akajizuia na uchafu huo na akataka hifadhi kwa Allah .

Na faida tunayopata hapa pia Allah -aliyetukuka- hakulitaja jina la huyu mwanamke kwa kumuhifadhi ,na katika qurani hakuna mwanamke aliyetajwa kwa jina isipokuwa Mariamu na hekima ya hilo ni kusisitiza na kutilia nguvu kuwa Isa -amani iwe juu yake- ni mtoto wa Mariamu na wala si mtoto wa Allah ,na hii ni kawaida ya waarabu huwa wanamstiri mno mwanamke mpaka wakawa hawataji majina ya wanawake ila kukiwa na haja kama vile yalivyotajwa majina mbali mbali ya maswahaba wa kike- Allah awaridhie-,

Vile vile tunajifundisha kuwa mtu anatakiwa ajitahidi asimfanyie ubaya yule aliyemfanyia wema ,kama alivyofanya Nabii Yusuf -amani iwe juu yake- alijiepusha na kufanya machafu na huyo mwanamke kwa sababu katika hilo kuna kuvunja mipaka ya Allah ,na pia ni kumfanyia ubaya yule ambaye amemfanyia ihsani na kumuandalia makazi mazuri.

Muandaaji: fawaidusalafiya.net
Tembelea website yetu: ☟
https://www.fawaidusalafiya.net
Telegram bonyeza hapa: ☟
https://t.me/fawaidussalafiyatz

🗓️ Imeandaliwa: Dhul-Qaadah 11, 1442H ≈ June 21, 2021M.

Muhimu: Vuna thawabu kwa kusambaza faida hizi. Sambaza kama ilivyo, si ruhusa kubadilisha chochote. Tuwe waadilifu.

Jiunge na chennel yetu ya telegram upate faida nyingi, kujiunga bonyeza link hii: 👇🏾
https://t.me/fawaidussalafiyatz

https://t.me/fawaidussalafiyatz
     •┈┈┈┈•✿❁✿•┈┈┈┈•

Comments

No comments yet. Why don’t you start the discussion?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *